Saturday, July 15, 2017
Channel Ten yalaumiwa kwa Kumuonyesha Paul Makonda
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limesema uamuzi wa pamoja wa kutotangazwa kwa habari zozote zinazomhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bado haujatenguliwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Katibu wa TEF, Neville Meena, amesema licha ya mkuu huyo wa mkoa kutangazwa mara kadhaa na vyombo vya habari, msimamo wa wahariri nchini kutotangaza habari zake bado haujatenguliwa.
Amesema vyombo vya habari vinavyomtangaza Mkuu huyo wa Mkoa kama vile Star TV and Channel ten, vinafanya hivyo kwa kukiuka msimamo wa pamoja ambao ulifikiwa na wahariri, wakiwamo wa vituo hivyo.
“Tunafahamu kuwa Mkuu wa Mkoa huyo ametangazwa zaidi ya mara moja katika kituo cha Channel Ten, mara moja katika tukio la msiba lililorushwa na kituo cha Radio cha EFM,” amesema Meena.
Amesema TEF haishangazwi na hatua hizo kwa sababu imekuwa ni msimamo wa vyombo vinavyomilikiwa na kampuni ya Sahara media (Star TV na Redio Free Afrika), ingawa wanachokifanya kikapingana na makubaliano ya ushirikiano wa kitaaluma (Professional Solidarity). Amesma uongozi wa TEF unalifanyia kazi suala hilo.
Amesema wameshaanza kuwasiliana na taasisi husika na baada ya hapo itatolewa taarifa rasmi kuhusu matokeo ya mchakato huo.
Meena amewakumbusha wahariri na waandishi wa habari kwamba makubaliano yaliyofikiwa kuhusu suala hili yako palepale hadi uamuzi mwingine utakapotanaghzwa.
“Tunaomba tuendelee kushirikiana katika kulinda uhuru wa taaluma yetu… hatufanyi hivi kwa kumchikia mtu, bali kulinda taaluma,” amesisitiza.
Amesema mtu ambaye amefungiwa kutokutangazwa habari zake ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na siyo habari za Mkoa wa Dar es Salaam kama baadhi ya watu wanavyosema.
“Kumfungia Mkuu wa Mkoa haimaanishi kuwa habari zote za mkoa wa Dar es Salaam zisizomhusisha mkuu huyo wa mkoa nazo zimefungiwa. Zitaendelea kutangazwa na kuandikwa kama kawaida,” amefafanua na kuongeza:
“Siyo kweli kwamba kutotangazwa kwa taarifa zinazomhusu Mkuu wa Mkoa ni kutotangazwa kwa habari za Mkoa. Huu ni upotoshaji unaofanywa kwa lengo la kuficha uovu ambao mhusika aliufanya kwa kuvamia chombo cha habari usiku akiwa na silaha.”
Source Udaku special blog
GAZETI HURU TZ
Maoni Yako Hapa Chini
Labels:
MATUKIO
No comments:
Post a Comment