Hatua 12 za kukuongoza katika kupanga malengo yako ni kama ifutavyo:
1: Fanya uamuzi wa dhati kutoka ndani wa kuamua unachokitaka kwenye kila eneo la Maisha yako.
Jiulize ni nini unachotaka kwenye kila eneo la maisha yako? Anza kwa kuweka uamuzi wa dhati wa mambo unayotaka yatokee na kufanyika kwenye maisha yako. Hebu anza na kujenga picha halisi ndani yako kuwa, kama mtu aliyepata nafasi ya kuwa na fedha za kutosha, marafiki wazuri, mtandao mkubwa wa mahusiano, elimu na uzoefu wa kutosha wa kukamilisha malengo yako binafsi. Jenga picha hiyo ili kuweza kuleta msukumo ndani yako wa kukupeleka katika kuchukua hatua katika malengo yako utakayojiwekea.
Weka picha halisi katika kila eneo unalohitaji kufanikiwa na kuleta matokeo chanya na makubwa juu yake. Mfano mzuri, jiulize kuwa:
- Kwanza: Unataka kuwa nani na kuwa wapi miaka mitano ijayo kutokea sasa? Weka malengo ya nafasi unayotaka kuwa miaka hiyo mitano hapo badae. Kama ni kupanda cheo kazini au ofisini kwako, kama ni kupata safari za nje, nakadhalika.
- Pili: Unataka uwe na aina gani ya familia? Unataka uwe na watoto wanagpi? Unataka usihi wapi wewe na familia yako? Weka malengo yahusuyo familia ili kuandaa familia iliyo bora hapo badae. Jambo hili si kwa watu wenaotaka kutengeneza familia tu bali hata kwa wewe uliye tayari na familia ni vizuri uwe na malengo ya kifamilia. Kwa mfano ni vizuri ufahamu unataka watoto wako wasome shule za aina gani na za gharama za kiwango gani?
- Tatu: Unataka kuongeza kiwango gani cha mapato yako katika biashara au kazi unayoifanya? Weka malengo yako ya mapato unayotaka kufikia.
- Nne: Unataka kumiliki kiasi gani cha mali au utajiri kiujumla (net-worth) katika maisha yako? Weka malengo ya kiwango cha mali unazohitaji kumiliki kutokea sasa.
“Setting goals is the first step in turning the invisible into the visible.”
– Tony Robbins
2: Ni muhimu kuandika malengo yako.Malengo yako ni muhimu sana yawe katika hali ya uandishi. Huwa napenda sana kusema jambo lolote ili liweze kufikia hatua ya utekelezaji ni lazima liwekwe katika mfumo wa maandishi. Unapochukua jukumu la kuandika malengo yako unasaidia akili yako kuwajibika dhidi ya malengo husika. Ni muhimu sana malengo yako yawe wazi, yanayoeleweka na yanayopimika. Unapoandika malengo yako inakusaidia kuona umbali (distance) ya lengo husika na rasilimali zinazohitajika juu ya lengo lako.
Utafiti unaonyesha ni asilimia 3% ya watu wazima walio na tabia ya kuandika malengo yao na kuwajibika kwa ajili ya kuyatimiza. Ni vizuri nikushauri ujiunge na asilimia 3% ya watu hawa ili kugeuza maisha yako kuwa kwenye nafasi ya ushindi leo hii. Kimbia asilimia 97% iliyoamua kuishi kwa mazoea na kutokuwa na nia ya dhati ya kufanikiwa.
3: Muda wa kufikia malengo yako.
Hebu nikupatie mfano mzuri katika jambo hili. Piga picha ndani yako umeamua kununua nyumba kwenye shirika la nyumba la taifa (NHC) halafu wasikupatie muda au tarehe maalum ya kukukabidhi nyumba yako, na zaidi sana unapowauliza watakupatia lini wanaishia kukupa jibu kuwa usubiri tu watakukabidhi nyumba yako. Nikuulize swali utajisikiaje ndani yako na tayari wewe umelipia nyumba yako na unauhitaji wa kuamia humo?
Nataka nikumbie wazi ndivyo ilivyo katika eneo au suala zima la kujiwekea malengo. Pasipo muda muafaka wa kutimiza au kufikia malengo yako ni rahisi sana kuishi ilimaradi tu pasipo kuruhusu akili yako kuwajibika ipasavyo ndani ya muda ulionao. Kuweka muda au tarehe ya kufikia malengo yako (deadline) ni muhimu sana ili kuisaidia akili yako iweze kuwajibika kila aiku na kuilazimisha kufuata kile ulichokipanga.
Na kama lengo lako ni kubwa zaidi, ni vizuri uligawe kwenye vipande vidogo vidogo ili uweze kulifanyia kazi hatua kwa hatua hadi litakapokamilika. Na kama kutatokea sababu yoyote itakayokufanya usikamilishe malengo yako ni vizuri uweke tarehe mpya ya kufikia lengo hilo.
4: Orodhesha vikwazo unavyoona vinaweza kuwa kizuizi cha kutimiza malengo yako.
Jiulize swali hili. Ni vizuizi au sababu gani zinazoweza kuwa kikwazo kwenye lengo halisi niliojiwekea kulitimiza? Tukitumia kanuni ya 80/20 tunaweza kusema; 80% ya vizuizi vya kufanikisha malengo yako vinatoka kwako binafsi, sababu kama vile kukosa ujuzi na maarifa ya kutosha, hofu na mashaka ya kujaribu. Ni 20% tu inayotoka nje ya maisha yako binafsi ikiwa kama fedha unazohitaji, watu wa kukusaidia, nakadhalika. Hivyo siku zote anza na wewe binafsi.
5: Weka wazi kwa kuandika ni maarifa gani, taarifa na ujuzi gani unaohitaji ili kukamilisha malengo yako.
Kama una ndoto ya kuwa mfanyabishara mkubwa, ni vizuri ufahamu ni ujuzi gani unaohitaji ili kuweza kukusadia kuwa bora katika eneo la kufanya biashara zako. Kwa kawaida mfanyabiashara yoyote yule anahitaji elimu ya kuuza, uongozi, kupanga bajeti, nakadhalika. Jiulize ni ujuzi gani ambao unahitaji ili uweze kukusaidia kuwa bora zaidi na miongoni mwa watu wenye uwezo mkubwa katika eneo lao la taaluma waliyonayo. Ni ujuzi gani nikiwa nao unaweza kuwa msaada mkubwa katika kukamilisha malengo yangu na kuleta matokeo makubwa katika maisha yangu?
6: Changanua katika akili yako ni watu gani unaowahitaji wanaoweza kuwa msaada mkubwa katika kukamilisha malengo yako.
Andika na kuorodhesha watu unaowajua na unaoweza kuanzisha mahusiano nao kuanzia sasa (networking) ili waweze kuwa msaada mkubwa katika kufikia malengo yako. Hakuna mtu anayeweza kufanikiwa kwa kufanya kila kitu peke yake. Unahitaji watu fulani katika maisha yako ili waweze kuwa msaada mkubwa wa wewe kutimiza ndoto na malengo yako uliyonayo. Wapo watu wanaotaka kuwekeza kwako, tafuta watu hao.Wakati mwingine ili kuweza kutimiza haja yako ya kuwa na watu fulani wanaoweza kukusaidia maishani mwako, inakubidi uwe ni mtu wa kujitolea kwa ajili yao. Jifunze kuwa mtoaji zaidi, hii itakusaidia kutengeneza mahusiano (networking) na watu wengi. Jiulize muda huu una nini ambacho ukikitoa kama vile maarifa uliyonayo, kutumia kipaji chako, fedha, nakadhalika, kinaweza kurudisha faida kubwa kwako hapo badae.
Kufanikiwa katika malengo makubwa tuliyonayo inatubidi tupate msaada kutoka kwa watu wengi waliotuzunguka. Hii ndio sababu ya watu wengi waliofanikiwa duniani kupenda kutengeneza mahusiano na watu wengi zaidi ili kuweza kupata masaada zaidi na kuongeza nafasi kwako ya kuafanikiwa.
“Be a “go-giver” rather than a “go-getter.”
-Brian Tracy
Unaweza kutizama malengo yako na kuangalia yanahitaji ufanye nini ili kuweza kuyafikia, baada ya kupata majibu orodhesha mambo yote uliyopata na vizuri uyaweke kama majukumu utakayochukua kila siku kwa kutekeleza moja baada ya jingine ili kuweza kufikia malengo yako uliyojiwekea. Chukua vikwazo ulivyovipata ukichanganya na maarifa na ujuzi unaohitaji, tumia kwa pamoja kama njia mojawapo ya kutimiza na kufikia malengo yako. Kama kikwazo chako ni hofu, tumia hofu kama fursa ya kuchukua hatua pasipo kuijali na kuiskiliza. Ukipata jambo jipya ni vizuri uliongeze katika orodha yako kama jukumu lingine la kutekeleza.
8: Pangilia orodha yako ya majukumu uliyonayo kwa njia ya kuweka vipaumbele.
Ndio. Ni vizuri upangilie majukumu yako yote uliyoorodhesha katika mpangilio maalum ukianzia jambo lenye uzito wa juu wa kutekeleza kwa haraka hadi la mwisho unaloweza kutekeleza hapo badae baada ya mengine. Kwa mfano, ni vizuri ujiulize maswali haya; Ni jambo gani ninaloweza kuanza kufanya kabla ya mengine niliyonayo? Ni jambo gani lililo la muhimu na lenye uzito kulitekeleza kabla ya yote? Na jambo gani lisilo na uzito ninaloweza kulitekeleza hapo badae baada ya kumaliza lile lenye umuhimu?
Kanuni 80/20 inasema kuwa, “80% of result will come from 20% of your activities.” (asilimia 80% ya matokeo unayoyapata yanatoka katika asilimia 20% ya majukumu au shughuli zenye uzito wa juu unazozifanya kila siku). Hivyo basi, ni muhimu sana uzingatie kufanya mambo machache lakini yenye uzito na yenye kuweza kuleta matokeo makubwa katika kutimiza malengo na ndoto yako uliyonanyo. Usifanye kila kitu kwani kufanya kila kitu ni kuchagua kufeli katika kila kitu.
9: Gawa vipaumbele vyako kwenye vipande vidogo vidogo ili kukamilisha kwa uharaka.
Kumbuka kila unapoweka malengo yako kisha ukamua kuweka vipaumbele vyako, hii inakuongezea nafasi kubwa ya kusogea mbele kwa haraka zaidi na utaokoa muda mwingi uliokuwa ukipoteza hapo nyuma katika kutekeleza majukumu yako. Utafiti unaonyesha kadiri mtu anavyotumia muda wake mwingi katika kupanga majukumu yake ya kufanya mbele yake, inamsaidia kutekeleza majukumu hayo kwa kutumia muda mdogo sana hasa pale anapoanza kuchukua hatua kivitendo.
Kanuni hii inasema kwamba, kila dakika moja unayoitumia kupanga unakuwa unaokoa dakika kumi za kutekeleza kile ulichokipanga. Hii inamaana kwamba mtu anayepanga kila mara ana faida ya kuokoa asilimia 1000% ya muda wake kila siku, wiki na mwezi. Je, kwa nini na wewe husiwe na tabia hii ya kupanga majukumu yako na kuweka vipaumbele vya majukumu uliyonayo ili kuokoa muda wako mwingi kwa ajili ya kuutumia kwa mambo mengine? Uamuzi ni wako, anza kupanga leo.
10: Chagua jambo la kwanza na muhimu kila siku katika orodha yako ya majukumu uliyonayo.
Jiulize swali kuwa; Je, ni jambo gani ninaloweza kulifanya kutoka katika orodha yangu ya majukumu niliyonayo linaloweza kuwa la kwanza kabla ya mengine niliyonayo? Unapomaliza kuangalia na kuchagua jambo la kwanza kisha ni vizuri zaidi uchague jambo lingine la pili unaloona na lenyewe lina uzito wa juu kwa ajili ya kulitekeleza, fanya hivyo hadi utakapomaliza majukumu yote uliyonayo katika orodha yako ili kuleta matokeo katika maisha yako.
Mara kwa mara zidi kujiuliza swali ni jambo gani lililo na thamani kubwa na linaloweza kuzaa matunda au kuleta matokeo makubwa katika maisha yako kwa siku uliyonayo, chagua jambo hilo kisha amua kulitekeleza hadi lilete matokeo unayoyataka maishani mwako. Kikubwa ni vizuri uzingatie umuhimu na uzito wa jambo husika kisha weka hatua za kivitendo kwa ajili ya kulitekeleza.
11: Weka tabia na nidhamu ya kukamilisha jambo moja kabla ya kuamia jambo lingine.
Tayari umechagua jambo mojawapo la kufanya ili kukamilisha sehemu ya majukumu yako uliyonayo. Tumia muda wako mwingi katika kufanya na kutumika katika jambo moja hadi ufanikiwe kabla ya kuamia jambo lingine (focus and committ on one course until you successfully). Uwezo wako wa kufanya jambo moja hadi kulikamilisha itakupa nafasi nzuri na kukusaidia katika kufanya mambo kwa ufanisi na umakini mkubwa kwa ajili ya kuleta matokeo mazuri kwenye malengo yako.
Kufanya jambo moja pekee ni sehemu mojawapo yenye nguvu kubwa ya kulinda muda wako ulionao. Hii ikiwa na maana kwamba utakuwa unaepuka muda mwingi uliokuwa unapoteza kwa kufanya kila kitu ulichoona kinafaa kufanyika. Pia itakusaidia kuwa na tabia ya kukamilisha majukumu yako uliyonayo pasipo kuishia kati, utaongeza nafasi ya kupata muda mzuri wa kuanza mapema kufanya mambo mengine kwa uharaka zaidi.
12: Jenga picha ya utayari wa kufanikiwa juu ya malengo yako.
Hatua ya mwisho ni kujenga picha iliyo wazi ndani yako katika akili, hisia na mawazo yako kuhusu mafanikio unayotaka juu ya malengo yako uliyojiweka. Ona ndani yako kama umekwisha kufanikiwa juu ya malengo yako uliyonayo. Kwa mfano kama ulikuwa na lengo la kuwa na gari, ni vizuri uanze kuona ndani yako unaendesha gari lako unalolitaka, haijalishi ni aina gani ya gari. Kama una lengo la kuishi kwenye nyumba yako nzuri anza kuona ndani yako unaishi kwenye nyumba hiyo kuanzia sasa.
Kila unapojenga picha ya kitu unachokitaka katika maisha yako unakuwa unatengeneza nafasi kubwa kwenye akili yako ya kuamini kufanikiwa katika kile kitu unachokitaka. Jenga picha hiyo ili kukupa msukumo ndani yako wa kusogea mbele zaidi katika kukamilisha lengo unalotaka kwa haraka zaidi. Sheria ya mvutano (the law of attraction) inasema, “kila unachoaminisha akili yako na kukiwaza kwa muda mrefu, unasababisha kitokee na kuvutwa kwa karibu na haraka zaidi katika hali ya nje ya maisha yako.” Unapoanza kuwaza jambo unalotaka kufanikiwa kama mtu aliyefanikiwa unasababisha watu kuvutiwa kwako, mawazo mazuri na rasilimali za kutosha kwa ajili ya kukusaidia kufanikiwa katika malengo yako kwa haraka.
Imeandaliwa na John Jonas Kiwovele
No comments:
Post a Comment