Kama
uliwahi kuandaa tangazo na kulitoa kwa watu ukijaribu kutafuta wateja,
mwitikio ukawa kidogo sana kuliko hata mategemeo ya kawaida, kuna
uwezekano ulifanya uchaguzi usio sahihi wa tangazo lililotakiwa kutumika
au ulilenga watu ambao sio wadau wa biashara au huduma yako.
Mfano,
unauza madela unazungukia vijiwe au maeneo wanayoishi na kufanyia kazi
wanaume, ukitarajia wanaume ndio wanunue wapelekee wake zao, hapo
utatumia muda mwingi lakini mauzo yatakuwa kidogo.
Kwa nini usifikie wanawake watumiaji na walihitaji wenyewe kabisa wa madela na ukauza kwa kiwango kikubwa?!
Katika
biashara ndogo au kubwa ukiweza kubaini walengwa wa biashara au huduma
yako, na ukatumia njia nzuri ya kufikisha huduma yako, utafanikiwa
katika biashara.
Hapa nimekuandikia njia 10 za kisasa za kutangaza biashara yako....
1.Jitambulishe/Watambulishe wengine– Wenzetu katika
lugha ya Kiingereza wanaita kitu hiki “networking”. Kwa bahati mbaya,
Kiswahili hakina neno mbadala la moja kwa moja kuhusu “networking” hii.
Kwa kifupi, ni kwamba ukiwa na biashara, kila unayekutana naye anaweza
kuwa mteja wako.Jitambulishe bila aibu.Mjue na yeye akujue, mwambie
unachokifanya(biashara yako).Pia usisahau marafiki zako.Je marafiki zako
wanajua unachokifanya? Watu wengi huwa wanasahau kwamba marafiki
wanaweza kuwa chanzo kizuri sana cha mauzo au kuongezeka kwa idadi ya
wateja.Waambie marafiki zako na wao(hususani kama ni marafiki kweli)
bila shaka watawaambia marafiki zao pia.
2.Kuwa na tovuti (website)– Katika zama za leo,ni
muhimu kwa biashara kuwa na tovuti. Natambua kwamba sio biashara zote
zinaweza au zina uwezo wa kuwa na tovuti. Unachotakiwa hapa ni wewe
mwenyewe kujiuliza, je aina hii ya biashara niliyonayo inahitaji uwepo
wa mtandaoni kupitia tovuti? Ni swali na jibu ambalo wewe mwenyewe
sharti ulipatie majibu. Uzuri wa tovuti au uwepo wa mtandaoni ni kwamba
hata pale biashara yako inapokuwa imefungwa(usiku kwa mfano kwa biashara
za mchana) bado unakuwa unaendelea kuitangaza.
3.Mitandao Jamii Ni Lazima– Sidhani kama natakiwa
kusisitiza zaidi jinsi gani ni muhimu kutangaza huduma au bidhaa zako
kupitia mitandao jamii kama vile Blogs, Facebook,Twitter,LinkedIn,Google
Plus etc. Kama unapenda kuandika,kwa mfano, anzisha blog.Andika,weka
video za huduma unazozitoa.Siku hizi kamera nyingi zina uwezo wa
kuchukua video.Kwanini usijichukue video ya dakika mbili ukielezea
bidhaa au huduma unazozitoa na kutuma mtandaoni kupitia mitandao jamii?
Bila shaka marafiki zako watakupata vizuri zaidi na wao wanawapelekea
wengine video hiyo.Ujumbe utaenea.
4.Orodhesha Biashara Yako katika Huduma Za Orodha Za Biashara–
Hatua muhimu katika biashara ni kutambulika. Njia mojawapo nzuri ya
kuchukua au kufikia hatua hii ni pamoja na kujiorodhesha. Kwa
mfano,biashara yako inahusiana na mazao ya kilimo.Kama kuna
umoja/ushirikiano wa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo hakikisha kwamba
jina lako na la biashara yako yanakuwepo katika orodha hiyo. Pia katika
nchi mbalimbali zipo huduma za kujiorodhesha zinazoitwa Kurasa Za
Njano(Yellow Pages). Hakikisha kwamba biashara yako ipo ndani. Pia
search engines kama vile Google,Yelp,Yahoo,Bing nk zinazo huduma
mbalimbali za kuorodhesha biashara mbalimbali katika nchi. Itumie fursa
hiyo. Angalizo: Katika kujiorodhesha kuwa makini,zipo huduma za Bure na
Za Kulipia.Kazi Ni Kwako.
5.Tumia Barua Pepe Kutangaza/Kujitangaza-Siku hizi
watu wengi wana e-mail address(anuani pepe). Bila shaka hata wewe
msomaji unayo.Kwanini basi usiitumie hiyo anuani pepe kuwasiliana na
wateja wako?Anapokuja kwenye sehemu yako ya biashara,muombe mteja anuani
pepe yake ili panapokuwa na “deal” umtumie.Mara nyingi hakuna
atakayekataa. Kila mtu anapenda “deal”.Ukishakuwa na anuani pepe,kwanini
usimkumbuke mteja wako aidha kwa “deal” au kumtumia e-card ya X-mas,Eid
nk? Angalizo: Usiwatumie wateja wako mambo mengi mengi mara kwa mara.Wanaweza dhani ni spammers na hivyo waka-block kabisa barua pepe kutoka kwako.
6.Gawa Business Cards– Niliwahi kusikia kisa cha
jamaa fulani ambaye alitengeneza business cards nzuri sana. Alipoona ni
nzuri sana akagoma kuzigawa.Akawa anaenda nazo kwenye mikutano nk lakini
hazigawi.Unajua kilichotokea? Biashara ikafa akabaki na business cards
zake.Nnachotaka kusema ni kwamba kila fursa inapojitokeza,gawa business
cards zako.Na usigawe tu na kutosema kitu.Mwambie kwa maneno machache
yule unayempatia business card kuhusu biashara yako. Muombe na yeye
akupe business card yake kama anayo. Kwa maneno mengine ukifanya hili
unakuwa pia umefanya lile nililolizungumzia mwanzoni kabisa.
7.Shiriki Katika Huduma/Shughuli za Kijamii– Kama
mfanyabiashara,njia mojawapo rahisi ya kuifanya jamii ikutambue ni
pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazoendelea katika
jamii. Unaweza kushiriki kama mdhamini au mfanyakazi wa kujitolea. Mara
nyingi huduma/shughuli hizi za kijamii huwa zinahudhuriwa na watu wa
habari(media) na kwa maana hiyo unaweza kuwa umepata “matangazo bila
kulipia”. Lakini cha muhimu zaidi ni kwamba unaposhiriki katika shughuli
za kijamii ni ishara kwamba unaijali jamii hiyo. Unapofanya hivyo ni
rahisi na wewe kuungwa mkono na wana jamii hao.
8.Muombe Mtu(mwandishi,blogger,mtangazaji nk) afanyie mapitio(review) bidhaa yako–
Utaratibu huu bado haujaingia sana nchini kwetu.Lakini mimi binafsi
naukubali sana. Kama unauza bidhaa fulani na unaamini kwamba bidhaa yako
ni bora,utafaidika sana endapo mtu kama mwandishi,blogger,mtangazaji wa
televisheni,radio nk,atakapoitumia bidhaa yako,kuona matokeo yake na
kisha kwenda hewani na kuwaambia wanaomsikiliza kuhusu bidhaa
aliyoitumia. Naomba nisisitize hapa kwamba ni muhimu akawa ameitumia
kweli na kupata matokeo anayoyapigia debe.Kinyume chake ni kwamba yeye
ataharibu heshima yake na wewe utakuwa umekosa lundo kubwa zaidi la
wateja. Angalizo: Kuna waandishi au bloggers na watangazaji nk ambao
hawafanyi mapitio BURE..Ongea nao muelewane.
9.Hudhuria na Tumia Vizuri Maonyesho Ya Biashara/Mikutano-Sio
kila biashara inaweza kushiriki katika maonyesho ya biashara hususani
yale makubwa kama vile Saba Saba au Nane Nane.Lakini yapo maonyesho
mengine mbalimbali(mfano kupitia wizara za serikali au umoja fulani wa
wafanyabiashara). Kila inapowezekana,usilaze damu.Shiriki.Pia shiriki
mikutano mbalimbali inayoandaliwa kwa ajili ya wafanyabiashara fulani.
Kwa uzoefu wangu,mikutano ya aina hii ipo na inafanyika mara kadhaa tena
bila malipo.Shiriki.Unapokwenda huko beba kadi zako za
biashara,vipeperushi nk.Gawa,ongea na wenzako,toa mchango na mawazo
yako.
10.Tangaza Kwenye Magazeti,Televisheni,Radio,Blogs Nk:
-Miongoni mwa njia/mbinu zote nilizozitaja hapo juu,pengine hii ndio
ikawa ya gharama zaidi. Lakini ukweli ni kwamba matangazo,yanalipa kwa
maana ya kwamba,kama uwezo upo,basi angalia uwezekano wa kutangaza
kupitia njia hizi. Lakini kitu kimoja ambacho ni vizuri kukizingatia
hapa ni kwamba unapoamua kutangaza kupitia njia hizi,kuwa
mbunifu.Usifanye tu kile ambacho washindani wako wa kibiashara
wanafanya. Jaribu kuwa na mawazo huru na binafsi. Pasua kichwa,fikiri.
Imeandaliwa na John Jonas Kiwovele
No comments:
Post a Comment