Saturday, July 15, 2017
Ufanye Nini Unapokatishwa Tamaa - Jifunze kupitia hadithi hii...
Kila mmoja wetu katika hatua fulani za maisha yetu huwa tunafikia sehemu ambayo kama vile tunataka kukata tamaa.Bila kujali tunafanya kazi ya kuajiriwa,tunajiajiri,tunafanya biashara,tunalima n,k kila mmoja wetu kuna wakati huwa anapitia hali hii kwenye maisha yake.Ila kitu cha msingi ni kuwa ili uwe mmoja wa wachache ambao watafanikiwa kumaliza hadi mwisho wa mashindano ni lazima ufanye kiapo cha kumaliza ulichokusudia hadi pale utakapopata suluhisho bila kukata tamaa yoyote.
Moja ya mtu ambaye ameshawahi kunisisimua na kunipa hamasa ya kutafuta ninachokitaka na kuhakikisha kuwa nimekipata ni mwanariadha anayeitwa Derek Redmond.Mwaka 1992 katika mashindano ya olimpiki ya Barcelona alikuwa anafanya jaribio lake la pili kutimiza ndoto yake ya kushinda katika mashindano ya olimpiki.Hii ni kwa sababu mwaka 1988 katika mashindano ya olimpiki ya Seoul,korea alipata jeraha na alilazimika kushidnwa kuendelea.Baada ya hapo alifanyiwa upasuaji wa mara kadhaa na alikuwa tayari amepona na kila mtu alimuona ndiye mtu ambaye atakuja kushidna mashindano ya olimpiki ya mita 400 jijini Barcelona.
Mashindano yalipoanza alifanikiwa kuvuka robo fainali na kisha akafika hadi nusu fainali.Alianza nusu fainali vizuri na alikimbia takribani mita 150 kabla hajapata tatizo la msuli wa paja na akaanguka chini akiwa na maumivu makali sana.Baada ya kuwa chini kwa sekunde kadhaa akawa kama amekumbuka kitu fulani na akainuka na akaendelea na mashindano.Kwa sababu ya maumivu alishindwa kukimbia vizuri na akaanza kuchechemea kwa kujilazimisha.Wakati anaendelea wenzake walikuwa wameshafika mwisho na wamemaliza mbio lakoini Dereki hakukubali kuishia njiani,alichotaka ni kuhakikisha kuwa amemaliza.
Baada ya muda alitokea mzee mmoja ambaye aliwasukuma askari na akaenda mpaka Derek alipokuwa na akamwambia “Derek huna haja ya kuendelea kukimbia” na Derek akamwambia “Ni lazima nimalize mashindano haya”-Huku akiwa bado anachechemea na anaugulia maumivu.Baba yake aliamua kumsaidia kwa kumuweka mkono mmoja begani na kuchechemea naye hadi mstari wa kumalizia ambapo alimaliza.Kukiwa na watazamaji 65,000 walisimama na kumuonyesha heshima kubwa sana.Ingawa Derek alihesabiwa kuwa hakushinda lakini ukweli ni kuwa alimaliza kwa namna bora zaidi ya yoyote Yule aliyekuwa katika mashindano yale.
Derek anatufundisha mambo mengi sana.Moja ni kuwa katika kuelekea kutimiza malengo tuliyonayo ni lazima tutakutana na changamoto amabzo zitatupa maumivu sana ambayo hatukuyatarajia.Ingawa Derek alikuwa amefanya maandalizi ya kutosha na kila dalili ilionekana atashinda lakini hali iligeuka na kuwa tofauti kabisa.Hii inaweza kutokea kwa mtu yoyote Yule;uanweza kujikuta umeingia katika tatizo ama changamoto ambayo hukuitegemea kabisa katika maisha yako yote.Unachotakiwa kujifunza kutoka kwa Derek ni kuwa hakukubali kukata tamaa kwa sababu ya changamoto na maumivu ambayo alikutana nayo kwenye maisha yake,aliendelea mbele.
Na wewe pia ni lazima uamue kua bila kujali umekutana na changamoto ya namna gani katika kuelekea kutimiza malengo yako,bila kujali unakutana na maumivu ya jinsi gani,ni lazima ufike mwisho wa kile unachokitafuta kwenye maisha yako.
Jambo la pili na la muhimu ni kuwa kama utaamua kuendelea mbele wakati bado uansikia maumivu na unaona kama umepata kikwazo cha kufanikiwa-Kuna msaada utakutokea mahali ambapo haukutarajia ili kukusaidia utimize lengo lako.Watu wengi sana huwa hawawezi kabisa hata kuvumilia kwa siku moja zaidi wanapokikuta kwenye tatizo fulani.Unachotakiwa kuelewa ni kuwa kama utaamua kuvumiliwa kwa kiwango fulani kidogo zaidi,kutakuwa na msaada utakuja kwako kutoka mahali ambapo haukutarajia.Msaada umeandaliwa kwa ajili ya watu ambao wako tayari kuvumilia kidogo zaidi.
Leo fanya maamuzi kuwa katika chochote kile ambacho unakitafuta kwenye maisha yako basi hautakuwa tayari kuishia njiani.Kama ambavyo kulikuwa na watu 65,000 wanasubiri Derek amalize;na wewe tambua kuwa kuna watu wengi sana ambao wanakusubiri ufanikiwe katika hiko unachofanya.Kuna maelfu ya watu maisha yao yatapona kama wewe pia utafanikiwa,Usifanye tu kwa ajili yako,fanya pia kwa ajili ya wengine.Nami nakusubiri pia utimize malengo yako ili nikushangilie.
Source:@JoelNanauka
©GAZETI HURU
johnkiwovele125@gmail.com
Labels:
DARASA
No comments:
Post a Comment