Naamini kuna wanawake ambao wanahisi kwamba hawawezi kufanya
kitu, wanachodhani kwamba wamezaliwa kwa ajili ya kuhangaikiwa,
hawaamini kwamba kama nao watajituma kwenye kufanya kazi, kupanua mawazo
yao kibiashara wataweza kufanikiwa.
Kuna wengine nao
wanahisi kwamba hata kama watapambana, bado watabaki palepale kwa kuwa
tu kuna watu nyuma wanawavuta. Kama una mawazo hayo, ndugu yangu utakuwa
unakosea sana kwani kuna wanawake waliopambana na kupata pesa na sasa
hivi ni mabilionea wakubwa duniani.
Leo ninakuletea
orodha ya wanawake weusi kama wewe ambao wamepambana sana na mwisho
wa siku kuwa mabilionea wakubwa, hawakujidharau, walijua kwamba
wanaweza kufanikiwa na hivyo kupambana sana na mwisho wa siku kupewa
heshima kila walipokuwa.
1.Isabel dos Santos
Unapowazungumzia
wanawake weusi wenye pesa duniani basi bila shaka mwanamke huyu atakuwa
mtu wa kwanza kuja kichwani mwako. Ni mtoto wa rais wa Angola, Jose
Eduardo dos Santos, ni mwanamke ambaye alianza kuzikusanya pesa tangu
kipindi kirefu nyuma, akafungua maduka makubwa, vituo vya televisheni,
ana migodi ya dhahabu. Anasema kwamba kila pesa anayoipata huwa
anaiingiza kwenye mzunguko kwani ukikaa nayo ni lazima utaifanyia
matumizi mengine yasiyokuwa na maana.
Ametoa ajira
nyingi nchini Angola lakini pia ameingia ubia na kampuni nyingi za Ureno
kama Nova Cimangola inayoshughulika na utengenezaji wa saruji, kampuni
ya simu ya Telefonica na kampuni nyingine nyingi nchini humo. Utajiri
wake ni dola bilioni 3.3 ambazo ni zaidi ya shilingi trilioni 7.
2. Oprah Winfrey
Ni mwanamke mweusi
Mmarekani mwenye umaarufu mkubwa duniani, anaendesha kipindi chake cha
Oprah Winfrey Show. Maisha yake ya nyuma yanasikitisha, hakuzaliwa
kwenye familia yenye pesa, alikuwa masikini mkubwa ambaye aliishia
kubakwa na kupata mimba utotoni.
Katika kupambana
kwake, aliwahi hata kukataliwa katika kituo cha televisheni kwa
kuonekana hajui. Ila kwa kuwa alidhamiria kupambana usiku na mchana,
mwisho wa siku akafanikiwa kwa kuanzisha kipindi chake nchini Marekani
ambacho kimekuwa kikiangalia dunia nzima.
Ingekuwaje
kama angekubalia kwamba yeye hajui? Ingekuwaje kama angekata tamaa baada
ya kukataliwa? Angefika hapo alipokuwa? Wakati mwingine hutakiwi kukata
tamaa hata kama mambo yatakuwa magumu kiasi gani. Sasa hivi ana utajiri
wa dola bilioni 3 ambazo ni zaidi ya trilioni 6.
3. Folorunsho Alakija
Ni mwanamke mwenye pesa nyingi kuliko wanawake wote nchini Nigeria. Katika
maisha yake ya ujanani, hakuwa na ndoto za kuwa bilionea mkubwa,
alipanga kuwa mwanamitindo na ndicho kitu kilichompeleka nchini
Uingereza.
Ila huko, akafanikiwa na hivyo kuamua
kujiingiza katika biashara mbalimbali. Akawekeza kwa wanamitindo, akawa
na kampuni kubwa ya uchapishaji na alipoona amepata pesa zaidi akaingia
katika uuzaji wa mafuta na kufungua kampuni yake ya Famfa Oil Limited
ambayo ndiyo ulimpa pesa zaidi.
Kwa sasa si mwanamitindo
tena, anapambana katika uuzaji wa mafuta nchini Nigeria, biashara
ambayo imemfanya kunukia pesa na kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa mpaka
kufikia utajiri wa dola bilioni 2.1 ambazo ni zaidi ya shilingi
trilioni 4.2
4. Sheila Crump Johnson
Ni Mmarekani
mwenye pesa ndefu, ndiye mmiliki wa Kituo cha Televisheni cha BET nchini
humo. Kwa kuwa alikuwa na pesa, aliamini kwamba kama angekuwa na vitega
uchumi mbalimbali basi angeingiza pesa zaidi.
Leo hii,
anamiliki timu za mpira wa kikapu nchini humo, Washington Wizard na
Washington Mystics, anamiliki hoteli kubwa ya Blue Ridge Mountains. Ni
mwanamke ambaye kichwa chake kinafikiria pesa kila siku, si mwanamke wa
kukaa na kusema kwamba wenzake wanafanikiwa lakini yeye hana bahati.
Unapoamua kupambana, huwezi kubaki hivyohivyo ulivyo kwani Mungu
ataangalia juhudi zako, ataangalia jasho lako na kukufungulia mlango wa
mafanikio. Sheila anamiliki utajiri wa dola milioni 710 ambazo ni zaidi
ya shilingi trilioni 1.4.
Itaendelea........... USIKOSE!!!
Source: Eric Shigongo
No comments:
Post a Comment